Kanisa halipaswi kuazima mitindo ya
kiganga kuendesha huduma za maombezi. Mitindo ya kiganga ni pamoja na matumizi
ya misamiati inayotumika kwenye anga za wapunga pepo, pamoja na kutumia
Askofu
Sylvester Gamanywa.
|
uzoefu wa kiganga/kichawi mtu aliuokuwa
nao kwenye ulimwengu wa giza na kuuleta katika huduma za kikanisa.
Hatari ya kuendekeza hii hali ni
kuanguka kwenye mitego wa Ibilisi wa kujaribu kudhoofisha utendaji halisi wa
nguvu za Roho Mtakatifu. Kumbuka Yule aliyekuwa Mchawi alivyotaka kununua
uwezo/karama ya kuwekea watu ujazo wa Roho Mtakatifu ili autumie kwenye uzoefu
wa kichawi aliokuwa kiufanya na kushangaza wengi huko Samaria.
Kama sio Petro kupitia karama ya
maarifa kumgundua hila zake si ajabu hata kama asingepokea fedha lakini angemkubalia
kuifanya huduma ya kuombea watu Roho Mtakatifu na badala ya watu kujawa na Roho
Mtakatifu wangejazwa “roho mtakafujo”!
Kwa hivi sasa, sio siri kwamba,
tayari wako watu waliojiingiza katika huduma za maombezi kwa madai ya
kuwafungua watu katika vifungo vya majini lakini miitndo inayotumika katika
huduma hizo inaonesha dalili zote za “wapunga pepo” wanaotumia uzoefu wa
kiganga/kichawi. Utawatambuaje? Ziko dalili za waziwazi kama Yesu alivyotabiri:
“Mtawatambua kwa matunda yao.”:
Wanajiita watumishi wa Mungu lakini
tabia na mienendo yao haina maadili ya utumishi wa Kristo. Wamejaa mizaha na
utovu wa nidhamu usioambatana na utendaji wa huduma za kweli zinazomwakilisha
Kristo katika utumishi.
Kipaumbele sio kuwafundisha watu
kumjia na kumjua Kristo na kuishi maisha ya utakatifu wa kweli. Wanachojali ni
kuteneza wafuasi wengi wataoendelea kuwa na “imani tegemezi” kwao; badala ya
kuwafundisha watu kumtegemea Kristo ambaye kimsingi ndiye mwenye mamlaka kamili
ya kuwafungua na kuwaweka watu huru mbali na vifungo vya pepo wachafu.
Mara nyingi kipambele katika huduma
ni kukusanya fedha kwa visingizio vya “jumbe zi kinabii” lakini zenye
kuambatana na malipo kama kigezo cha kufunguliwa kwa wagonjwa na wenye pepo.
Hii ndiyo ile ya Yule Simoni mchawi akiyeingiza suala la “kununua karama ya
Mungu kwa mali” ili apate kuifanyia biashara katika maombezi
Kanisa
halipaswi kupokea na kufanyia kazi
ushauri
wa mapepo katika maombezi
Hili ni onyo kwa watumishi wa kweli
wanaofanya huduma za maombezi, lakini pasipo kujua au kukusudia, wamejikuta
wametumbukia katika mtego wa kutegemea taarifa zinazotolewa na mapepo
yaliyowapagaa watu zinazodai sababu za kuwapagaa na nini kifanyike ili
wawaachie waliowapagaa.
Watumishi wa kweli wa Kristo,
hawapaswi, kwa namna yoyote ile; kupokea na kufanyia kazi ushauri wa mapepo
kama ndio mtindo na njia ya watu waliopagawa wapate kufunguliwa!
Kwa kusema hivi sina maana kwamba
pasiwepo kabisa mawasiliano na pepo wanapowapagaa watu. Ninachomaanisha ni
kwamba wakati wa “mawasiliano na pepo”, ajenda kuu iwe ni “kuyakemea na
kuyaamuru yatoke kwa mamlaka ya Kristo pasipo kutafuta kuwa na muafaka wa
masharti ya mapepo”!
Uchunguzi na uzoefu nilioupata
katika utumishi huu wa huduma za maombezi, ninao ushahidi wa kutosha
kuthibitsha kwamba, sio wote wanaopagawa na pepo wakati wa maombezi hufunguliwa
mara moja. Wengine huchukua muda kutokana na mfumo wa maisha wanayoishi,
ufahamu duni wa Neno la Mungu, na utayari wa kujitoa kikamilifu kuishi maisha
ya utakatifu kama yasemavyo maandiko.
Kwa hiyo mapepo kupiga kelele na
kuangusha watu chini wakati wa maombezi; kisichukuliwe kuwa kigezo pekee kwa
wahusika wanafunguliwa. Kufunguliwa katika pepo kwa walio wengi ni mchakato
ambapo wahusika wanatakiwa kutoa ushirikiano makini ikiwa ni pamoja na kuhimizwa
kupokea wokovu wa Yesu Kristo, na utayari wa kupitia mafundisho makini ya Neno
la Mungu na, utayari wa kubadilika kitabia na mwenendo kama njia ya
kufunguliwa kikamilifu.
Mungu
alikwisha kutoa mamlaka
ya
kudhibiti uchawi kanisani
Ni wakati wa kanisa sasa kurejea
kwenye ufunuo wa kanisa la kwanza na kuwa na mamlaka ile ambayo Kristo
aliwakabidhi mitume wake kama ilivyoandikwa:
“Akawaita wale Thenashara, akawapa
uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. (LK. 9:1)"
Katika makala yaliyopita tulifunza
kupitia maandiko haya kuhusu neno hili “Uwezo” kwa kiyunani linaitwa “Dunamis”
lenye kumaanisha “nguvu ya kutenda miujiza ya uumbaji, au kuharibu nguvu za
pepo wabaya”! Kwa hiyo, Yesu Kristo alipowapa wanafunzi wake “uwezo na mamlaka”
juu ya pepo wote, maana yake aliwapa nguvu za kufukuza au kutoa pepo wabaya
watoke ndani ya watu wengine bila mjadala!
Pia tuliwahi kujifunza kwamba Bwana
Yesu alipoagana na wanafunzi wake, aliwaahidi kupokea hii nguvu ya “dunamis”
mara tu Roho Mtakatifu atakapowashukia.
“Lakini mtapokea nguvu (dunamis) akiisha kuwajilia juu yenu Roho
Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu kuanzia Yerusalemu, uyahudi wote,
Samaria hata mwisho wa nchi.” (Mdo.1:8)
Mwisho kabisa, tunauoa utendaji wa
mamlaka ya kupambana na kuvunja shughuli za uganga/uchawi kila mahali ambapo
Injili ya Kristo ilipohubiriwa:
“Na watu wengi katika wale
waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya
watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha
hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa
nguvu.” (MDO 19:19, 20)
Maandiko haya yanashuhudia jinsi
kanisa la kwanza lilivyotamba dhidi ya nguvu za uchawi na kuleta maelfu katika
ufalme wa Mungu. Huu ndio uamsho unaohitajika makanisa wa kuendesha huduma za
maombezi yenye mamlaka halisi ya nguvu za Roho Mtakatifu na kuonesha matokeo ya
kufunguliwa kikamilifu kwa wote wanaomjia Kristo.
Haifai kabisa kanisa kuendelea
kuongozwa na ushauri wa mapepo ambao huwajengea hofu waamini badala ya ujasiri
wa kutoa pepo. Kumbuku Yesu Alisema “ishara hizi zitafuatana na hao waaminio
kwa jina langu watatoa pepo” na sio “Hofu ya uchawi itafuatana na hao waaminio
nao watapunga pepo”!?
Mwisho
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni