20 Nov 2014

                       Maana ya wokovu

Wokovu ni kazi ya Mungu kwa ajili yetu (1Tim 2:4; 2Tim 1:9-10). Sisi hatuwezi kujikomboa, lakini Mungu ana nguvu kuliko shetani na mabaya yote, naye anatuhurumia sisi maskini (Kol 1:13-14). Alifanya nini ili kutuokoa? Ndiyo historia ya wokovu. Wapo walioiandika katika Biblia ili tusadiki na kuishi upya (1Pet 1:10-12). Humo mtu hatazamwi kama nafsi ya peke yake tu, bali zaidi kama mtu wa taifa lake; hivyo Mungu anatangazwa kuwa hashughulikii wokovu wa mtu binafsi tu, bali wa mataifa mazima pia, kuanzia lile la Israeli. Aliyowatendea wao ni hasa kuwatoa utumwani Misri, kuwapa agano na masharti yake li awafanye taifa huru katika nchi bora. Waisraeli walijenga imani yao juu ya hayo mang’amuzi ya msingi ya wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, halafu wakajikumbusha kwamba alikuwa ameshawaahidia mababu wao baraka kama hizo. Hatimaye tu walitafakari juu ya asili ya watu na ya ulimwengu, wakaelewa kuwa Mungu aliweza kuwaokoa kwa sababu ndiye aliyeumba vyote: hakuna wa kushindana naye na wa kuzuia mpango wake kwa ajili ya watu. Kwa Wakristo tukio kuu lililo msingi wa imani ni ufufuko wa Yesu, aliyetoka kaburini mzima na mtukufu, wa kwanza kati ya umati, akaingia katika nchi ya walio hai kweli.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni